‘Chomoka na Mwananchi’ yavutia maelfu
Wafanyakazi wa Kampuni ya Mwananchi Communications Ltd waliotengeneza
umbo la ‘M’ (Mwananchi) kuashiria kuanza kwa promosheni kabambe ya
kuwajaza wasomaji wake mamilioni ya fedha na magari matatu mapya. Picha
na Emmanuel Herman
endelea........
Kwa ufupi
Hata hivyo, wafanyakazi na wauzaji wa magazeti ya Mwananchi hawaruhusiwi kushiriki shindano hilo.
Dar es Saam. Mkurugenzi Mtendaji wa Mwananchi Communications Limited (MCL), Tido Mhando amesema Promosheni ya Chomoka na Mwananchi iliyoanza jana, imepokewa kwa mikono miwili na maelfu ya wasomaji wa gazeti hilo kote nchini.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Mhando
alisema wasomaji walijitokeza kwa wingi na kuanza kushiriki promosheni
hiyo jana asubuhi, shughuli waliyoendelea kuifanya mpaka jioni.
“Hii inamaanisha kuwa hata kwenye maeneo ambayo
gazeti linachelewa kufika, pia watu wameshiriki. Naomba nisisitize tu
kuwa lengo letu ni kuwashukuru wananchi kwa kuendelea kusoma gazeti
letu,” alisema Mhando.
Pamoja na maelezo hayo, Mhando alitoa angalizo kwa
wauza magazeti kuwa nao kama walivyo wafanyakazi wa MCL, hawaruhusiwi
kushiriki katika promosheni hiyo na kuwa kufanya hivyo ni kosa kisheria.
“Watakaobainika na kukamatwa kwa kukiuka utaratibu huu watachukuliwa hatua za kisheria,” alisema.
Aliongeza kuwa baadhi ya wauzaji hawa wamekuwa
wakichukua namba za magazeti na kuzituma, kisha kuwauzia wateja gazeti
husika na pale wanapojaribu kutuma namba iliyo kwenye gazeti wanaambiwa
kuwa tayari imeshatumika.
“Wanachofanya ni kujisumbua, ikumbukwe kuwa ili
mtu uwe mshindi na upewe zawadi yako ni lazima uwe na gazeti zima la
Mwananchi ambalo namba yake ndiyo uliyoituma, gazeti hilo ndiyo risiti
yako, kama huna huwezi kupata zawadi kwa hiyo hata wasomaji nawataka
wahakikishe wanahifadhi magazeti yao kwa kipindi chote cha promosheni,”
alisema Mhando.
Meneja Masoko wa MCL, Bernard Mukasa alisisitiza
umuhimu wa kuhifadhi nakala za magazeti yote kwa washiriki wa promosheni
hiyo na kuwataka kusoma na kuelewa vigezo na masharti ya promosheni
hiyo, ambavyo vimekuwa vikichapishwa kwenye gazeti la Mwananchi.
“Mtu ambaye hatakuwa na gazeti ama aliyetumia
gazeti lisilo lake, hatuwezi kumpa zawadi, lakini pia niwashukuru
wasomaji wetu kwa kushiriki kwa wingi promosheni hii, tangu asubuhi
tumekuwa tukipokea simu za wateja wakitaka ufafanuzi wa mambo
mbalimbali,” alisema Mukasa.
Juzi, MCL ilizundua promosheni iliyopewa jina la
Chomoka na Mwananchi ambapo wasomaji wataweza kujinyakulia fedha
tasilimu Sh100,000,000 na magari mapya matatu, vyote vikiwa na thamani
ya Sh250,000,000.
Akizindua promosheni hiyo ambayo itafanyika nchini
kote kwa siku 100 kuanzia juzi, Mhando alisema kila siku kutakuwa na
mshindi wa Sh1,000,000.
“Hii ni promosheni ambayo lengo lake ni
kuwashukuru wasomaji wetu kwa kuendelea kulipenda gazeti lao na kuliweka
juu nchini,” alisema.
No comments:
Post a Comment