Ponda asimamisha shughuli Morogoro
Sheikhe Ponda Issa Ponda akiwa chini ya ulinzi wa askari magereza wakati
akielekea katika mahakama ya hakimu mkazi Morogoro kusikiliza kesi yake
inayomkabili.
Kwa ufupi
Morogoro.
Kiongozi wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu, Sheikh Ponda Issa Ponda jana alisababisha kusimama kwa shughuli za Serikali wilayani Morogoro baada ya ofisi kadhaa ikiwamo ya Mkuu wa Wilaya na baadhi ya mitaa kufungwa ili kupisha kusikilizwa kwa kesi inayomkabili katika Mahakama ya Mkoa wa Morogoro.
Kiongozi wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu, Sheikh Ponda Issa Ponda jana alisababisha kusimama kwa shughuli za Serikali wilayani Morogoro baada ya ofisi kadhaa ikiwamo ya Mkuu wa Wilaya na baadhi ya mitaa kufungwa ili kupisha kusikilizwa kwa kesi inayomkabili katika Mahakama ya Mkoa wa Morogoro.
Tofauti na Agosti 19, mwaka huu wakati
aliposafirishwa kwa helikopta, jana Sheikh Ponda alisafirishwa kwa
barabara kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro akiwa chini ya ulinzi.
Mbali ya Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Morogoro
kufungwa, nyingine ni Hazina Ndogo, Madini, Posta, Vipimo, Ukaguzi na
Maktaba ya Mkoa.
Sababu za kufungwa kwa ofisi hizo pamoja na Mtaa
wa Stesheni na maeneo ya Posta ni kuwa jirani na Mahakama hiyo. Magari
yalizuiwa kutembea katika njia na maeneo ya karibu na ofisi pamoja na
Mahakama hiyo huku kukiwa na idadi kubwa ya askari polisi na magereza
kwa muda wote wa takriban saa mbili.
Alifikishwa mahakamani hapo saa 4:10 asubuhi akiwa
katika basi la Magereza ambalo lilisindikizwa na jingine dogo, huku
magari mengine yakisimamishwa kupisha msafara huo. Mahakama hiyo
ilifurika umati wa wafuasi wa kiongozi kiasi cha kuwalazimu polisi na
wana usalama wengine kuweka utepe kuwazuia wengi wao kufika katika jengo
lililokuwa likitumika kuendesha kesi hiyo.
Shughuli katika eneo hilo zilirejea katika hali
yake ya kawaida saa 6:25 mchana baada kesi yake kuahirishwa na msafara
wa Sheikh Ponda kurejea katika Gereza la Segerea, Dar es Salaam ambako
yuko rumande.
Muda wote tangu kuwasili mpaka kusikilizwa kwa
kesi hiyo, wafuasi hao walikuwa kimya hadi pale ilipoahirishwa na hasa
baada ya Sheikh Ponda kuwapungia mkono alipokuwa akielekea kwenye basi
ambako walisikika wakisema: “Takbriir na kuitikia Allahu Akbar – (Mungu
Mkubwa).”
Kesi yenyewe
Katika kesi hiyo, Wakili wa Serikali, Benard
Kongola alisema mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Mkoa wa Morogoro,
Richard Kabate kuwa Sheikh Ponda alitenda makosa ya uchochezi Agosti 10,
mwaka huu saa 11.45 jioni kwenye maeneo ya Kiwanja cha Ndege, Morogoro.
Alisema siku hiyo, Sheikh Ponda alialikwa kutoa
maelezo machache kwenye Kongamano la Eid lililoandaliwa na Umoja wa
Wahadhiri Mkoa wa Morogoro (Uwamo) na kwamba akiwa hapo alitamka maneno:
“Ndugu Waislamu, msikubali uundwaji wa kamati za ulinzi na usalama za
misikiti kwani kamati hizo zimeundwa na Baraza la Waislamu Tanzania
(Bakwata), ambao ni vibaraka wa CCM na Serikali na kama watajitokeza
kwenu watu hao na kujitambulisha kwamba wao ni kamati za ulinzi na
usalama za misikiti, fungeni milango na madirisha ya misikiti yenu na
muwapige sana,” huku akijua kutoa maneno hayo ni kosa kisheria.
Alisema kwa kufanya hivyo, Sheikh Ponda
anayetetewa na mawakili watatu wanaoongozwa na Juma Nassoro, alivunja
masharti ya Mahakama ya kifungo cha nje iliyotolewa na Mahakama ya
Hakimu Mkazi Kisutu ya Mei 9, mwaka huu iliyokuwa imetamka kuhubiri
amani.
Katika shtaka la pili, Sheikh Ponda anadaiwa
kuwashawishi wafuasi wake kutenda kosa la jinai kwa kuwaambia: Serikali
ilipeleka jeshi Mtwara kushughulikia suala la vurugu iliyotokana na gesi
kwa kuwaua, kuwabaka na kuwatesa wananchi kwa sababu asilimia 90 ya
wakazi wake ni Waislamu, lakini haikufanya hivyo kwa wananchi wa
Loliondo waliokataa Mwarabu asipatiwe kipande cha ardhi ya uwindaji
baada ya kudai ni mali yao kwa sababu asilimia 90 ya wakazi wake ni
Wakristo.” Shtaka la tatu ni kudaiwa kutamka maneno yaliyoumiza imani ya
watu wengine kama yalivyo katika shtaka la pili.
No comments:
Post a Comment