Pages

Saturday, 24 August 2013

‘Chomoka na Mwananchi’ yavutia maelfu


Wafanyakazi wa Kampuni ya Mwananchi Communications Ltd waliotengeneza umbo la ‘M’ (Mwananchi) kuashiria kuanza kwa promosheni kabambe ya kuwajaza wasomaji wake mamilioni ya fedha na magari matatu mapya. Picha na Emmanuel Herman 
endelea........

Kwa ufupi
Hata hivyo, wafanyakazi na wauzaji wa magazeti ya Mwananchi hawaruhusiwi kushiriki shindano hilo.


Dar es Saam. Mkurugenzi Mtendaji wa Mwananchi Communications Limited (MCL), Tido Mhando amesema Promosheni ya Chomoka na Mwananchi iliyoanza jana, imepokewa kwa mikono miwili na maelfu ya wasomaji wa gazeti hilo kote nchini.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Mhando alisema wasomaji walijitokeza kwa wingi na kuanza kushiriki promosheni hiyo jana asubuhi, shughuli waliyoendelea kuifanya mpaka jioni.
“Hii inamaanisha kuwa hata kwenye maeneo ambayo gazeti linachelewa kufika, pia watu wameshiriki. Naomba nisisitize tu kuwa lengo letu ni kuwashukuru wananchi kwa kuendelea kusoma gazeti letu,” alisema Mhando.
Pamoja na maelezo hayo, Mhando alitoa angalizo kwa wauza magazeti kuwa nao kama walivyo wafanyakazi wa MCL, hawaruhusiwi kushiriki katika promosheni hiyo na kuwa kufanya hivyo ni kosa kisheria.
“Watakaobainika na kukamatwa kwa kukiuka utaratibu huu watachukuliwa hatua za kisheria,” alisema.
Aliongeza kuwa baadhi ya wauzaji hawa wamekuwa wakichukua namba za magazeti na kuzituma, kisha kuwauzia wateja gazeti husika na pale wanapojaribu kutuma namba iliyo kwenye gazeti wanaambiwa kuwa tayari imeshatumika.
“Wanachofanya ni kujisumbua, ikumbukwe kuwa ili mtu uwe mshindi na upewe zawadi yako ni lazima uwe na gazeti zima la Mwananchi ambalo namba yake ndiyo uliyoituma, gazeti hilo ndiyo risiti yako, kama huna huwezi kupata zawadi kwa hiyo hata wasomaji nawataka wahakikishe wanahifadhi magazeti yao kwa kipindi chote cha promosheni,” alisema Mhando.
Meneja Masoko wa MCL, Bernard Mukasa alisisitiza umuhimu wa kuhifadhi nakala za magazeti yote kwa washiriki wa promosheni hiyo na kuwataka kusoma na kuelewa vigezo na masharti ya promosheni hiyo, ambavyo vimekuwa vikichapishwa kwenye gazeti la Mwananchi.
“Mtu ambaye hatakuwa na gazeti ama aliyetumia gazeti lisilo lake, hatuwezi kumpa zawadi, lakini pia niwashukuru wasomaji wetu kwa kushiriki kwa wingi promosheni hii, tangu asubuhi tumekuwa tukipokea simu za wateja wakitaka ufafanuzi wa mambo mbalimbali,” alisema Mukasa.
Juzi, MCL ilizundua promosheni iliyopewa jina la Chomoka na Mwananchi ambapo wasomaji wataweza kujinyakulia fedha tasilimu Sh100,000,000 na magari mapya matatu, vyote vikiwa na thamani ya Sh250,000,000.
Akizindua promosheni hiyo ambayo itafanyika nchini kote kwa siku 100 kuanzia juzi, Mhando alisema kila siku kutakuwa na mshindi wa Sh1,000,000.
“Hii ni promosheni ambayo lengo lake ni kuwashukuru wasomaji wetu kwa kuendelea kulipenda gazeti lao na kuliweka juu nchini,” alisema.


No comments:

Post a Comment