Watu 13 wafariki ajalini Kahama
Suleiman Kova
Kwa ufupi
Kahama.Watu 13 wamepoteza maisha papohapo
akiwamo mtoto mchanga wa miezi saba, baada ya gari walilokuwa
wakisafiria kugonga lori la mizigo lililokuwa limeharibika barabarani
katika Kijiji cha Ngongwa, wilayani Kahama, Mkoa wa Shinyanga.
Ajali hiyo ilitokea juzi saa 2:30 usiku wakati gari aina ya Toyota Hiace lilipoligonga lori.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Kihenya
Kihenya, alisema Hiace hiyo ilikuwa ikifanya safari zake kutoka mjini
Kahama kwenda mji mdogo wa Ushirombo, katika Wilaya ya Bukombe, mkoani
Geita.
Kihenya alisema watu 11 akiwamo dereva ambaye pia
ni mmiliki wa gari hilo, Ezekiel Werema, walifariki dunia papohapo na
wengine wawili walifariki dunia wakiwa katika Hospitali ya Wilaya ya
Kahama kwa matibabu.
Alisema polisi wanahangaika kutafuta majina ya marehemu na majeruhi, ili ndugu na jamaa zao waweze kutaarifiwa.
Pia, Kihenya aliwashukuru wananchi wa kijiji hicho
kwa ushirikiano walioonyeshwa kwa polisi baada ya ajali kutokea na
kuongeza kuwa, hadi sasa baadhi ya watu tayari wamejitokeza Hospitali ya
Wilaya ya Kahama kutambua maiti.
Kamanda Kihenya alisema chanzo cha ajali hiyo ni
mwendokasi, huku akitoa wito kwa madereva kuwa makini wanapoendesha
magari hasa nyakati za usiku.
Kwa upande wake, Kaimu Mganga Mfawidhi Hospitali
ya Wilaya ya Kahama, Dk Joseph Fwoma alithibitisha kupokea maiti 11
kutoka eneo la ajali na kwamba, majeruhi wawili walifariki dunia
wakipatiwa matibabu hospitalini hapo.
Wakati huohuo, Bakari Kiango anaripoti kuwa,
polisi Kanda katika Maalum ya Dar es Salaam, wanawashikilia watu wanne
wanaodhaniwa kuwa ni majambazi kwa tuhuma za kufanya uhalifu wakitumia
sare za JWTZ na JKT.
Akizungumza na waandishi wa habari, Kamanda wa
Polisi wa Kanda hiyo, Suleiman Kova alisema watuhumiwa hao walikamatwa
usiku wa kuamkia jana katika maeneo ya Temeke.
Alisema kukamatwa kwao kulikuja baada ya polisi
kupata taarifa kutoka kwa raia wema kuhusu watu hao kupanga kufanya
uhalifu. Hilo ni tukio la nne kutokea ndani ya Agosti mwaka huu.
“Tutakomesha tabia hii ya watu kutumia sare hizi
kwani imekuwa ikiwachanganya wananchi ambao wengi wao wakiwaona
watuhumiwa hawa wanajua ni askari wa ukweli kumbe ni wahalifu,” alisema
Kova.
No comments:
Post a Comment