Serikali yasalimu amri kwa Dowans
Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG),Fredrick Werema
Kwa ufupi
- Maswi alisema baada ya Waziri Muhongo kutoa kauli hiyo bungeni, utekelezaji wake unapaswa kufanywa na wanasheria wa Serikali na kwamba mtu sahihi wa kuulizwa ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) kwa sababu Tanesco ni shirika linalomilikiwa na umma kwa asilimia 100.ENDELEA....
Habari za uhakika zilizopatikana jana zinasema
hatua hiyo ya Serikali inatokana na ushauri ambao imekuwa ikipewa na
wanasheria wake kwamba “uwezekano wa kushinda kesi hiyo ni mdogo sana.”
Mvutano uliopo unatokana na Serikali kukata rufaa
kupinga uamuzi wa Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi (ICC), ambayo
iliipa ushindi Dowans Holdings ya Costa Rica katika kesi namba
15945/VRO.
Jana, Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati na Madini,
Eliakimu Maswi na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umeme Tanzania
(Tanesco), Felichesmi Mramba kwa nyakati tofauti walisema Serikali
ilikwishatangaza bungeni kwamba inakusudia kumaliza kesi zote ambazo
zimekuwa zikizorotesha mipango ya maendeleo.
“Sifahamu kwa upande wa kisheria wamefikia wapi
katika suala hilo (la Dowans), lakini niseme kwamba waziri wetu (Profesa
Sospeter Muhongo), alitangaza bungeni kwamba lazima tuondokane na kesi
ambazo zinatukwamisha, kwa hiyo kama wameanza majadiliano ni hatua
nzuri,” alisema Maswi.
Maswi alisema baada ya Waziri Muhongo kutoa kauli
hiyo bungeni, utekelezaji wake unapaswa kufanywa na wanasheria wa
Serikali na kwamba mtu sahihi wa kuulizwa ni Mwanasheria Mkuu wa
Serikali (AG) kwa sababu Tanesco ni shirika linalomilikiwa na umma kwa
asilimia 100.
Kwa upande wake, Mramba alisema: “Ninachofahamu ni
kwamba kuna maandalizi ya kuwezesha mazungumzo hayo kufanyika, kama
ulisikiliza hotuba ya bajeti ya mheshimiwa waziri (Muhongo), alisema
mpango wa Serikali ni kuondokana na kesi hizi.”
Awali, kulikuwa na taarifa kwamba Serikali
imewalipa Dowans kiasi cha Dola za Marekani 78 milioni (Sh124.8
bilioni), lakini Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa alikanusha taarifa
hizo akisema hakuna ukweli kuhusu jambo hilo.
Akizungumza kwa simu kutoka Sudan jana, Dk Mgimwa
alisema: “Kwa uelewa wangu hakuna malipo hayo, isipokuwa kwa masuala
mengine ya kisheria unaweza kuwasiliana na AG (Mwanasheria Mkuu wa
Serikali), nikirudi unaweza kupata taarifa zaidi.”
Hata hivyo, AG, Jaji Frederick Werema alipoulizwa
kuhusu suala hilo alisema Serikali haihusiki kwa namna yoyote na kesi ya
Dowans na kwamba wanaopaswa kufahamu kwa undani suala hilo ni wale
walioshtakiwa, akimaanisha Tanesco.
“Hiyo siyo kesi ya Serikali na haihusiki kwa namna
yoyote ile, kaangalie parties (wahusika) zinazotajwa kwenye hati ya
kiapo, hapo Serikali haipo bwana, kwa hiyo waulize wahusika wanaweza
kuwa na information (taarifa) zaidi,” alisema Jaji Werema.
Suala la kufanyika kwa usuluhishi nje ya Mahakama
pia nalo bado ni kitendawili kutokana na ukweli kwamba hata Kampuni ya
Uwakili ya Rex Arttoneys ambayo imekuwa ikisimamia kesi Dowans hapa
nchini, haifahamu kuwapo kwa mazungumzo hayo.
Mmoja wa Mawakili wa Kampuni hiyo, Dk Thomas Nguluma alisema
juzi kuwa hawafahamu chochote kuhusu mpango huo wa Serikali na kwamba
ikiwa umeanza kufanyika basi wao hawakuhusishwa.
“Sisi bado tuna mkataba na Tanesco, lakini kwa
hilo unalolisema kwa kweli kama lipo hatujahusishwa, kama tukihusishwa
basi hatutakuwa na haja ya kuficha chochote,”alisema Dk Nguluma.
Kesi ya Dowans
Katika madai yao, Dowans walikuwa wakitaka walipwe
kiasi cha Dola za Marekani 149 milioni kutokana na uzalishaji wa umeme
na gharama za kukatishwa kwa mkataba wake, lakini ICC iliwapa tuzo ya
kulipwa Dola za Marekani 65 milioni.
Wakati Dowans wakiwa kwenye mchakato wa kukazia
hukumu hiyo katika Mahakama Kuu jijini London, Uingereza, Tanesco
kupitia kwa mawakili wa Kampuni ya Matrix ya nchini humo waliwasilisha
maombi ya kutaka kuahirishwa kwa ukaziaji huo, kutokana na kufunguliwa
kwa kesi ya kuupinga katika Mahakama Kuu ya Tanzania.
Tangu wakati huo, Tanesco hawajawahi kushinda kesi
yoyote kati ya tatu ambazo zimewahi kujitokeza katika shauri hilo, huku
riba ya fedha wanazotakiwa kulipa kwa Dowans ikiwa watashindwa kesi,
ikiongezeka kila kukicha.
Kutokana na kesi ambayo ilifunguliwa katika
Mahakama Kuu na baadaye Mahakama ya Rufani hapa nchini, hivi sasa riba
imesababisha fedha zinazopaswa kulipwa kwa Dowans kukaribia Dola 120
milioni (zaidi ya Sh190 bilioni).
Serikali kupitia Tanesco pia ililazimika kuweka
dhamana ya Dola 31 milioni za Marekani (Sh50 bilioni) za dhamana
kutokana na kesi zilizofunguliwa hapa nchini kuchelewesha kukaziwa kwa
uamuzi wa ICC Uingereza.
No comments:
Post a Comment