Washtakiwa EPA jela miaka 13
Washtakiwa wa EPA, Bahati Mahenge (kulia), Manase Mwakale (katikati)
wakiwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam
jana, baada ya kuhukumiwa.Mahenge alihukumiwa kwenda jela miaka saba
wakati Mwakale akihukumiwa miaka mitano. Picha na Venance Nestory
Kwa ufupi
- Akitoa hukumu hiyo jana kwa niaba ya wenzake, Jaji Sekela Mushi na Sam Rumanyika,Msajili Lameck Mlacha alisema mshtakiwa Bahati Mahenge atatumikia kifungo cha miaka saba jela.
Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu
imewahukumu kwenda jela jumla ya miaka 13, washtakiwa watatu katika kesi
ya wizi wa Sh1.1 bilioni katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA).
Akitoa hukumu hiyo jana kwa niaba ya wenzake, Jaji
Sekela Mushi na Sam Rumanyika,Msajili Lameck Mlacha alisema mshtakiwa
Bahati Mahenge atatumikia kifungo cha miaka saba jela.
Mshtakiwa Manase Makale atatumikia kifungo cha
miaka mitano jela na mkewe ambaye ni mshtakiwa katika kesi hiyo, Edda
Makale atatumikia kifungo cha mwaka mmoja na nusu.
Washtakiwa wawili kwenye kesi hiyo iliyosikilizwa
kwa miaka mitano, Davis Kamungu na Godfrey Mushi waliachiwa huru baada
ya mahakama kuwaona hawana hatia.
Mbali na kutoa hukumu hiyo, aliamuru mshtakiwa
Bahati Mahenge na Manase Makale kurejesha kiasi cha Sh1,186,534,303.27
walichodaiwa kukiiba katika akaunti EPA,iliyopo Benki Kuu ya Tanzania
(BOT).
Akiendelea kusoma hukumu hiyo, Mlacha aliwaachia
huru washtakiwa Davis Kamungu na Godfrey Mushi baada ya kuwaona hawana
hatia kutokana na upande wa mashtaka kushindwa kuthibitisha pasipo
kuacha shaka mashtaka dhidi yao. Kabla ya hukumu hiyo kutolewa, Wakili
wa Serikali Mwandamizi, Shadrack Kimaro aliiambia mahakama kuwa upande
wa mashtaka hauna rekodi za uhalifu za washtakiwa hao.
Kimaro aliiomba mahakama kutumia mamlaka yake
chini ya kifungu cha 348(1) na cha 358(1) cha mwenendo wa mashauri ya
jinai sura ya 20 kuwaamuru washtakiwa waliotiwa hatiani kurejesha fedha
walizochukua na kuisababi+shia Serikali hasara.
“Mshtakiwa Mahenge, Manase na Edda wameonekana
wanahatia, makosa waliyoyafanya ni mazito yameiingizia nchi yetu hasara
kubwa, wapewe adhabu kali,” alieleza Wakili Kimaro mahakamani hapo.
Kwa upande wa mshtakiwa Mahenge aliiomba mahakama
impunguzie adhabu kwa sababu ana watoto wanne, wazazi wake ni wazee wote
wanamtegemea.
Alidai kuwa alikuwa akihudhuria kesi kwa miaka
mitano sasa toka mwaka 2008 ni kama alikuwa akitumikia kifungo hivyo
aliiomba mahakama ufikirie muda huo wakati ukitoa adhabu hiyo.
Manase Makale, yeye alidai kuwa ni mgonjwa
anafamilia kubwa inayomtegemea na mshtakiwa Edda Makale ni mkewe hivyo
kama wote watahukumiwa watoto wao watateseka.
Baada ya kutolewa kwa maelezo hayo, Hakimu Lameck
alisema katika shtaka la kwanza la kula njama washtakiwa Mahenge na
Makale walionekana wana hatia na watatumikia kifungo cha miaka mitano
jela.
No comments:
Post a Comment