JK azindua shule, x-ray Mwanza
Mwanza. Rais Jakaya Kikwete amefungua shule ya kisasa ya msingi
ya Ntulya Wilaya ya Misungwi, iliyotolewa zawadi kwa wanakijiji na
taasisi kutoka Marekani.
Pia, Rais Kikwete amezindua huduma za x-ray kwenye
Hospitali ya Wilaya ya Misungwi, siku yake ya kwanza ya ziara ya kikazi
ya siku tano mkoani Mwanza.
Shule ya Ntulya iliyoko kilomita 47 kutoka mjini
Misungwi, ina wanafunzi 466 na walimu 11 na ni zawadi ya Taasisi ya
Africa School House ya Marekani kwa wanakijiji cha Ntulya ambako
Mwanzilishi na Mkurugenzi wa taasisi hiyo, Dk Aimee Bessire ambaye
amehudhuria sherehe za uzinduzi wa shule hiyo na mume wake, Mark Bessire
walipata kuishi wakifanya utafiti kuhusu utamaduni wa Kabila la
Wasukuma.
Shule hiyo ya kisasa imejengwa kwa matofali ya
kuchomwa na ilijengwa kati ya 2008 na 2010. Ina madarasa 11, nyumba 10
za walimu na kisima cha maji safi. Kwa jumla shule hiyo ina uwezo wa
kuwa na wanafunzi 600 kwa wakati mmoja.
Akizungumza kwenye sherehe hizo, Dk Bessire ambaye
amezungumza kwa ufasaha lugha za Kiingereza, Kiswahili na Kisukuma,
alisema kuwa shule hiyo imejengwa kwa jumla ya Sh1.038 bilioni, na kati
ya hizo Sh980 milioni zilitolewa na Africa School House, Halmashauri ya
Misungwi ilichangia Sh28 milioni na nguvu za wananchi zilichangia Sh30
milioni.
Taasisi hiyo ya Marekani pia imewajengea
wanakijiji hao wa Ntulya, Kituo cha Afya kwenye eneo hilo la shule na Dk
Bessire alisema kuwa taasisi hiyo ina mipango ya kujenga shule ya mfano
ya sekondari ya bweni ya wasichana.
Dk Bessire pia alisema kuwa yataanzishwa madarasa kwenye shule hiyo kwa ajili ya watu wazima wasiojua kusoma na kuandika.

No comments:
Post a Comment