Pages

Wednesday, 9 October 2013

Wawekezaji wanyanyasaji kufukuzwa


SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema wawekezaji watakaobainika kujishughulisha na vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia pamoja na kuwasumbua wafanyakazi katika sekta za mahoteli watachukuliwa hatua za kinidhamu ikiwemo kufukuzwa nchini.

Hayo yalisemwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Haroun Ali Suleiman wakati akijibu swali la Mwakilishi wa Viti Maalumu Wanawake, Salma Mussa Bilali (CCM)aliyetaka kujua hatua zinazochukuliwa kwa wawekezaji wanaodhalilisha wafanyakazi wa nchini.
Bilali alisema katika ukanda wa hoteli za kitalii yapo malalamiko mengi kwamba wanawake wanafanyiwa vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia na viongozi wa hoteli hizo.
Akifafanua zaidi, Suleiman alisema Wizara ya Kazi na Utumishi tayari imeweka sheria za kazi kwa wawekezaji wa nje kuhakikisha kwamba wanaajiri wafanyakazi wazalendo.
Lakini alisema suala la udhalilishaji wa kijinsia pamoja na kuwasumbua wafanyakazi wazalendo limepewa kipaumbele cha kwanza ambapo mwekezaji atakayedhalilisha wafanyakazi kwa kuwafukuza bila ya kufuata utaratibu wa kisheria hatua za kinidhamu zitachukuliwa dhidi yao.
“Nataka niwahakikishie wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kwamba mwekezaji atakayebainika kuwadhalilisha wafanyakazi wazalendo na kuwafukuza kazi watachukuliwa hatua za kisheria,”alisema.
Suleiman alisema Wizara tayari imewachukulia hatua za kisheria zaidi ya viongozi wa hoteli za kitalii wapatao 10 na kuwanyang’anya vibali vya kufanya kazi nchini. Hata hivyo, Haroun aliwataka wafanyakazi wanaofanya kazi katika sekta ya Utalii na hotelini kufuata sheria na taratibu za kazi kwa ajili ya kuepuka vitendo vya udhalilishaji ikiwemo kupoteza ajira.
Alisema baadhi ya wamiliki wa hoteli za kitalii wametoa malalamiko yao kwa wafanyakazi wazalendo kwamba wamekuwa wakikiuka masharti ya sheria za kazi pamoja na kushindwa kufika kazini kwa wakati.
“Yapo malalamiko tumeyapokea kutoka kwa wamiliki wa hoteli za kitalii kwa wafanyakazi wazalendo...lipo tatizo la udokozi na kushindwa kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa sheria,” alisema.
Mapema Haroun alisema Serikali inawafuatilia wafanyakazi wa sekta binafsi ikiwemo za hoteli za kitalii kuhakikisha kwamba wanafunga mikataba na wafanyakazi wao na kupeleka michango ya mafao katika mifuko ya hifadhi ya jamii.
Haroun alisema hayo wakati akijibu swali la nyongeza la mwakilishi wa jimbo la Muyuni, Jaku Hashim Ayoub (CCM) aliyetaka kujua hatua zinazochukuliwa kwa waajiri sekta binafsi ambao wanashindwa kulipa michango kwa wafanyakazi wao katika mifuko ya hifadhi ya jamii.
“Tunawafuatilia waajiri wote ambao wanashindwa kulipa michango ya watumishi wao katika Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (ZSSF)...waajiri wasiopeleka michango yao tutawachukulia hatua za kisheria kwani ni kinyume na sheria za uajiri nchini," alisema.
Share/Bookmark

No comments: