Wabunge wastaafu walia njaa kwa Spika
OFISI ya Bunge inaangalia utaratibu wa
kufundisha wabunge ujasiriamali baada ya kubainika baadhi ya wanaokoma
kushika wadhifa huo, kukabiliwa na hali mbaya ya ukwasi na kulazimika
kuomba msaada.
Spika wa Bunge, Anne Makinda amesema maisha ya siasa kwa
sasa sio kazi ya kutegemea kwa sababu hawana mkataba na wananchi; hivyo
umefika wakati kuangalia jinsi ya kufundisha wabunge ujasiriamali
kuondokana na adha ya ukata mara ubunge unapokoma.
Akizungumza na Spika wa Bunge la Uswisi,
Maya Graf jijini Dar es Salaam jana, Spika Makinda alisema moja ya
changamoto inayokabili bunge hivi sasa ni kwamba wabunge hawana pensheni
baada ya ubunge kukoma. Alisema baadhi ya wabunge wamekuwa katika hali
mbaya kifedha mara wamalizapo kipindi chao cha ubunge.
“Kwa kweli hali ni mbaya, ni wakati sasa
umefika tutaanzisha programu ya kuwafundisha ujasiriamali wabunge, ili
wawe na kitu cha ziada cha kufanya, ili hata kama hatachaguliwa kwenye
awamu nyingine, asiwe kwenye hali mbaya kimaisha, awe na kitu cha
kufanya”, alisema Makinda.
Akifafanua hilo alisema siasa siyo kazi
ya kudumu kwa sasa, na kwamba hata wale wanaokosa nafasi ya kurudi
bungeni kwa awamu nyingine, huwa vigumu kupata ajira kwa kuwa hata
waajiri hudai hao ni wanasiasa.
Alisema, ubunge ni kazi ambayo mtu
anakuwa na mkataba na wananchi na kwamba kama wananchi wataamua
kutomchagua kwa mara nyingine, ndio mwisho wa ubunge hivyo ni vyema kuwa
na kazi mbadala kufanya maisha yaendelee.
Alisema ingawa ubunge ni kazi ambayo
haina pensheni baada ya mhusika kumaliza kipindi , lakini wanapokuwa
kwenye nafasi, fedha wanazopata huzitumia pia kwa ajili ya maendeleo ya
majimbo yao.
Mishahara ya wabunge Aidha, alisema
ingawa mishahara ya wabunge siyo mikubwa kama ilivyo kwa wabunge wa nchi
nyingine, hata kama ikiongezwa haitatosha kutatua matatizo
wanayokumbana nayo.
“Wakipatacho mara nyingine hukitumia pia kwenye majimbo yao kusaidia wananchi,” alisema.
Aliongeza, “Kwa kweli tuna changamoto,
nafasi ya ubunge haina pensheni mara ubunge unapokoma, tunapata kiinua
mgongo, sasa kama mbunge hakuchaguliwa tena kuendelea na nafasi hiyo,
kwa awamu nyingine baadhi yao wanakuwa kwenye hali mbaya.” Waomba mshiko
Aliongeza,
“hali ni mbaya, wapo wabunge wastaafu
unawaona unashituka, wengine wanafululiza hapa unawapa chochote
ulichonacho sasa, ili kuondokana na adha hii tunaangalia jinsi ya
kuwasaidia kabla ya kumaliza kipindi cha ubunge wawe na kazi au
biashara”.
Hata hivyo alisema hivi sasa wabunge
wengi ni vijana na kwamba kwa hali halisi ya kazi ya ubunge ni wazi
kwamba wenye uamuzi ni wananchi, hivyo ikiwa wanakosa kwa awamu
nyingine, na hawana kazi nyingine ya kufanya, hali itakuwa mbaya zaidi.
Akifafanua jinsi watakavyoweza kugawa
muda wa ujasiriamali na kazi ya ubunge, Makinda alisema katika programu
hiyo wataangalia pia jinsi ya kutenga muda ili kufanya mambo yote kwa
ufasaha na umakini. Rafu katika uchaguzi
Akizungumzia uchaguzi Makinda alisema,
chaguzi nyingi za ubunge zimekuwa za kufa kupona kwa wagombea kwa kuwa
wanafahamu ikiwa watakosa na hawana kazi nyingine, huo unakuwa mwanzo
mgumu wa maisha.
“Mnapogombea nafasi ya ubunge kwenye
majimbo ya uchaguzi unakuwa wa kufa au kupona kwa kuwa wengi wa wagombea
wameacha kazi au hawana kazi na kama watakosa nafasi hiyo basi hapo
ndio ugumu wa maisha unaanza”, alisema Makinda.
Kadhalika, alisema ili kuondoa migongano
na ugomvi mara baada ya uchaguzi kumalizika, ni vyema wabunge
wakafundishwa ujasiriamali ili kama akiwania nafasi na kushindwa kwa
haki asiwe na kinyongo na aliyeshinda, bali atafanya biashara kwa kuwa
ana elimu au mafunzo.
Spika wa Uswisi ashauri Kwa upande wake
Spika wa Uswisi, Maya Graf alisema mfumo wa Bunge la Tanzania na wa kwao
hautofautiani kwani wao pia kama mbunge hatachaguliwa kwa awamu
nyingine, hufanya kazi nyingine.
“Kwetu kupata kazi sio shida, ukiwania
nafasi ya ubunge ukakosa, unaweza kupata kazi kwa kuangalia fani
uliyonayo, hii ndio tofauti ya kwenu na kwetu, ila kupata ubunge ni
matakwa ya wananchi kama wanakukubali”, alisema Graf.
Aliongeza kuwa ni vyema changamoto hiyo
ya ajira au biashara mara baada ya ubunge kukoma ikaangaliwa na
kutafutiwa ufumbuzi, ili kuwasaidia wabunge waweze kuendelea na maisha
na kuondokana na umaskini.
No comments:
Post a Comment