Seif apongeza mkutano wa JK na vyama
MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar,
Maalim Seif Sharif Hamad, amempongeza Rais Jakaya Kikwete kwa kuzungumza
na vyama vya siasa kuhusu Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko
ya Katiba 2013, akisema ametumia njia sahihi kabisa.
Aidha, amesema itakuwa balaa kama Taifa
kwenda katika Bunge la Katiba wakati bado kuna mvutano, na pia kama
baada ya kupitishwa kwa Katiba, vyama vitaenda kwa wananchi kupiga
kampeni ya kuzuia Katiba mpya.
Maalim Seif alisema hayo jana wakati
akizungumza na waandishi wa habari mjini Unguja kuzungumzia miaka mitatu
ya utendaji wa Serikali ya Awamu ya Saba ya Zanzibar, ambayo ni ya
Umoja wa Kitaifa.
“Mimi nampongeza Rais Kikwete kwa
kufanya mazungumzo na vyama vya siasa. Ametumia njia sahihi kabisa,
nampongeza kwa asilimia mia moja,” alisema Maalim Seif na kuongeza:
“Itakuwa balaa kubwa sana kama
tutakwenda katika Bunge la Katiba, kukiwa bado kuna mvutano, au kwamba
baada ya Katiba kupita bungeni, vyama vitafanya kampeni ya kutaka Katiba
isipite. “
Alisema njia ya mazungumzo aliyoitumia
Rais Kikwete ndiyo mwafaka na pia maagizo yake kwamba vyama vyote
ikiwamo CCM wakae na kuzungumza, ni sahihi.
“Matarajio yangu ni kwamba vikao
vilivyofanyika na maazimio ya vikao hivyo, kati ya Rais na viongozi wa
vyama vya siasa, yatazaa maafikiano mema, ili hatua zinazofuata katika
suala zima la kuandika Katiba mpya ziendelee kwa amani na utulivu na
matarajio ya wananchi walio wengi yafikiwe,” alisema Maalim Seif ambaye
pia ni Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF).
Alisema Katiba lazima iwe shirikishi na
ibebe maoni ya watu wengi, na kwamba wapo watu ambao wanataka kuuvuruga
mchakato huo au kuifanya Katiba isiwe ya watu wengi, kwani suala hilo ni
la makubaliano zaidi.
Aidha, alimpongeza Rais Kikwete kwa
kuona umuhimu wa kuwashirikisha Watanzania wenyewe kuandika Katiba mpya,
na kuongeza kuwa la msingi zaidi ni kuwa wananchi washirikishwe
kikamilifu.
Mwanasiasa huyo mkongwe ambaye Oktoba
22, mwaka huu, alitimiza umri wa miaka 70, alisema ingawa alitoa maoni
yake kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba wakati ikikusanya maoni hayo,
chama chake hakina tatizo kwa sasa na Rasimu ya Katiba iliyotolewa maoni
na mabaraza.
No comments:
Post a Comment