Wawekezaji wanyanyasaji kufukuzwa
SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar
imesema wawekezaji watakaobainika kujishughulisha na vitendo vya
udhalilishaji wa kijinsia pamoja na kuwasumbua wafanyakazi katika sekta
za mahoteli watachukuliwa hatua za kinidhamu ikiwemo kufukuzwa nchini.
Hayo yalisemwa na Waziri wa Nchi Ofisi
ya Rais Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Haroun Ali Suleiman wakati
akijibu swali la Mwakilishi wa Viti Maalumu Wanawake, Salma Mussa Bilali
(CCM)aliyetaka kujua hatua zinazochukuliwa kwa wawekezaji
wanaodhalilisha wafanyakazi wa nchini.
Bilali alisema katika ukanda wa hoteli
za kitalii yapo malalamiko mengi kwamba wanawake wanafanyiwa vitendo vya
udhalilishaji wa kijinsia na viongozi wa hoteli hizo.
Akifafanua zaidi, Suleiman alisema
Wizara ya Kazi na Utumishi tayari imeweka sheria za kazi kwa wawekezaji
wa nje kuhakikisha kwamba wanaajiri wafanyakazi wazalendo.
Lakini alisema suala la udhalilishaji wa
kijinsia pamoja na kuwasumbua wafanyakazi wazalendo limepewa kipaumbele
cha kwanza ambapo mwekezaji atakayedhalilisha wafanyakazi kwa
kuwafukuza bila ya kufuata utaratibu wa kisheria hatua za kinidhamu
zitachukuliwa dhidi yao.
“Nataka niwahakikishie wajumbe wa Baraza
la Wawakilishi kwamba mwekezaji atakayebainika kuwadhalilisha
wafanyakazi wazalendo na kuwafukuza kazi watachukuliwa hatua za
kisheria,”alisema.
Suleiman alisema Wizara tayari
imewachukulia hatua za kisheria zaidi ya viongozi wa hoteli za kitalii
wapatao 10 na kuwanyang’anya vibali vya kufanya kazi nchini. Hata hivyo,
Haroun aliwataka wafanyakazi wanaofanya kazi katika sekta ya Utalii na
hotelini kufuata sheria na taratibu za kazi kwa ajili ya kuepuka vitendo
vya udhalilishaji ikiwemo kupoteza ajira.
Alisema baadhi ya wamiliki wa hoteli za
kitalii wametoa malalamiko yao kwa wafanyakazi wazalendo kwamba wamekuwa
wakikiuka masharti ya sheria za kazi pamoja na kushindwa kufika kazini
kwa wakati.
“Yapo malalamiko tumeyapokea kutoka kwa
wamiliki wa hoteli za kitalii kwa wafanyakazi wazalendo...lipo tatizo la
udokozi na kushindwa kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa sheria,”
alisema.
Mapema Haroun alisema Serikali
inawafuatilia wafanyakazi wa sekta binafsi ikiwemo za hoteli za kitalii
kuhakikisha kwamba wanafunga mikataba na wafanyakazi wao na kupeleka
michango ya mafao katika mifuko ya hifadhi ya jamii.
Haroun alisema hayo wakati akijibu swali
la nyongeza la mwakilishi wa jimbo la Muyuni, Jaku Hashim Ayoub (CCM)
aliyetaka kujua hatua zinazochukuliwa kwa waajiri sekta binafsi ambao
wanashindwa kulipa michango kwa wafanyakazi wao katika mifuko ya hifadhi
ya jamii.
“Tunawafuatilia waajiri wote ambao
wanashindwa kulipa michango ya watumishi wao katika Mfuko wa Hifadhi ya
Jamii (ZSSF)...waajiri wasiopeleka michango yao tutawachukulia hatua za
kisheria kwani ni kinyume na sheria za uajiri nchini," alisema.
No comments:
Post a Comment