Viongozi watoa ushuhuda Kulola alivyowasaidia
Mdhamini wa Makanisa ya EAGT, John Mfuko akitoa heshima za mwisho mbele
jeneza lenye mwili wa Askofu Mkuu wa Kanisa la Evangelistic Assemblies
of God Tanzania(EAGT), Dk Moses Kulola jijini Dar es Salaam. Picha na
Salim Shao.
Kwa ufupi
Dar es Salaam. Ibada ya kuaga mwili wa Askofu
Mkuu wa Kanisa la Evangelistic Assemblies of God Tanzania(EAGT), Dk
Moses Kulola (83) ilichukua sura mpya baada ya viongozi kadhaa wa
Serikali nchini, kufunguka na kutoa siri za mafanikio yao kwa maombi
yake ikiwemo kupata uwaziri.
Viongozi hao ni pamoja na Paul Kimiti ambaye
alikiri mbele ya maelfu ya waombolezaji kwamba maombi ya Askofu huyo,
yalimpa mafanikio makubwa ikiwa ni pamoja na kupata uwaziri mara mbili.
“Nakumbuka aliniombea tena ofisini kwangu wakati
huo nikiwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, mbele ya bendera za taifa
nilipiga magoti mbele ya mtumishi wa Mungu alikuwa anatembea na Yesu,
kweli kila goti litapigwa kwa Yesu, kwa maombi yake nilifanikiwa kuwa
waziri kwa vipindi viwili, ilibaki nusra niupate na uwaziri Mkuu,”
alisema Kimiti akifuatiwa na kelele za kushangiliwa.
Kimiti amewahi kuwa Waziri wa Ajira na Maendeleo ya Vijana na Waziri wa Kilimo na Biashara, kati ya mwaka 1995 na mwaka 2000.
Kwa upande wake, Mchungaji Getruda Rwakatare
ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalumu, alisema Askofu Kulola alikuwa ni
baba yake wa kiroho na kwamba alimtambua baada ya ndoa yake kuwa na
mgogoro.
“ Alinifariji sana, aliniombea nakumbuka kuna
wakati nilimweleza jinsi mateso yalivyoendelea katika ndoa yangu,
aliniambia kama mume wako anakupiga au kukutesa tambua hakutesi wewe
bali Yesu aliye ndani yako, maneno yale yalinitia nguvu nikabadilika
nikawa mtumishi wa Mungu hadi leo naye akawa ananiita nabii Debora,”
alisema Mchungaji Rwakatare.
Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, Advera Senso
akiwasilisha rambirambi ya Sh 2,000,000, alisema kuwa jeshi hilo
limepoteza kamanda wa kiroho na kimwili ambaye walikuwa wanamtumia
kutokana na mahubiri yake katika kuzuia matukio ya uhalifu ikiwemo ya
kikatili ya kukata viungo vya albino.
Makamu wa Askofu wa EAGT, Asumwisye Mwaisabila
akitoa salamu zake kwenye ibada hiyo, aliwataka viongozi wote wa
makanisa ya kiroho kumaliza tofauti zaoili kumuenzi Askofu Kulola ambaye
alikuwa na upendo wa pekee.
No comments:
Post a Comment