Pages

Thursday, 12 December 2013

Ni vilio vitupu A. Kusini



Mjane wa Rais wa Kwanza Mazalendo wa Afrika Kusini, Graca Machel akitoa heshima za mwisho kwa mwili wa mumewe katika Ikulu ya Pretoria nchini humo jana. Picha na AFP  

Pretoria: Familia ya Rais wa kwanza mzalendo wa Afrika Kusini, Nelson Mandela jana iliongoza utoaji wa heshima za mwisho kwa mwili wa kiongozi huyo, katika tukio ambalo limebadili mwelekeo wa maombolezo tangu alipofariki dunia, Desemba 5, mwaka huu.
Mjane wa Mandela, Graca Machel aliwaongoza wanafamilia katika Ikulu ya Pretoria waliposema ‘buarini’ kwa kiongozi huyo katika tukio ambalo mbali na kufungua pazia ya utoaji wa heshima za mwisho, liliibua simanzi miongoni mwa waliohudhuria.
Mandla ambaye ni mjukuu mkubwa wa Mandela, yeye alikuwa katika Majengo ya Umoja ilipo Ikulu tangu asubuhi na alikabidhiwa mwili kama kiongozi wa familia kutoka kwa Majenerali wa Jeshi la Afrika Kusini (SADF).
Mandla akionekana mwenye mawazo mengi na huzuni kubwa, kutwa nzima alikuwa ameketi pembezoni mwa jeneza lililokuwa na mwili wa babu yake, hadi ulipoondolewa Ikulu na kwenda kuhifadhiwa katika Hospitali ya Jeshi saa 11:30 jioni. Wakati familia ya Mandela ikiingia kuaga, jeneza lilikuwa wazi likiacha kioo pekee kilichokuwa kikiwatenganisha na mwili wa mpendwa wao.
Graca alikuwa hatua chache nyuma ya Rais Jacob Zuma na alipofika katika jeneza lenye mwili wa mumewe alisimama kwa sekunde chache akimtazama, kisha akaendelea. Nyuma ya Graca, alikuwa ni Mtalaka wa Mzee Mandela, Winnie Madikizela na mabinti zake wawili, pamoja na wanafamilia wengine, ambao baada ya kutoa heshima zao za mwisho, walionekana wakitumia lesso zao kufuta machozi. Familia hiyo ilifuatiwa na Rais Mstaafu, Thabo Mbeki na Frederick de Klerk ambao waliambatana na wake zao, lakini mke wa de Klerk, Elita alishindwa kujizuia na kuangua kilio.
Kulikuwa na simanzi kubwa miongoni mwa waombolezaji waliofika kutoa heshima zao za mwisho, wakati ambao Rais Zuma pia aliwaongoza viongozi wa nchi mbalimbali kumuaga Madiba.
Rais Jakaya Kikwete alikuwa miongoni mwa waliotoa heshima za mwisho akiungana na marais wenzake, wengi wakiwa kutoka Afrika ambao waliondoka jana mchana baada ya kupata fursa hiyo.
Miongoni mwao walikuwa marais wastaafu; Kenneth Kaunda wa Zambia na Joachim Chissano wa Msumbiji.
Marais wengine waliokuwapo na nchi zao kwenye mabano ni Robert Mugabe (Zimbabwe), Joyce Banda (Malawi), Uhuru Kenyatta (Kenya), Ellen Johnson – Sarlief (Liberia), Goodlucky Jonathan (Nigeria) na Michael Satta (Zambia).
Jeneza lenye mwili wa Mandela liliwekwa juu ya kizimba maalumu ambacho kilikuwa kimezungushiwa utepe wenye rangi nyekundu, huku ukiwa umefunikwa na kibanda cha rangi nyeupe kilichojengwa kwa ustadi mkubwa.
Walikuwapo askari wanne wa Kikosi cha Jeshi la Wanamaji wa Afrika Kusini wakizunguka jeneza hilo; wawili mwanzoni na wawili mwishoni, wakiwa wamevalia mavazi meupe, kushika kitara mkononi kila mmoja.

No comments: