Mansour: Nitazungumza baada ya uamuzi wa chama
Wajumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Mapinduzi wakijadiliana jambo kabla
ya kuanza kwa kikao kilichoongozwa na Mwenyekiti wa chama hicho, Rais
Jakaya Kikwete, mjini Dodoma jana. Kutoka kushoto Pindi Chana, Dk Maua
Daftari, Dk Asha-Rose Migiro, Salmin Awadh Salmin na Sophia Simba. Picha
na Edwin Mjwahuzi
Kwa ufupi
Taarifa kutoka ndani ya kikao cha kamati hiyo ambazo
Mansour amekiri kuzisikia zinaeleza kuwa uamuzi huo umetokana na yeye
kudaiwa kupingana na Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010, ambayo
inaunga mkono muundo wa serikali mbili.
Dar es Salaam. Baada ya Kamati Maalumu ya Chama
Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, kudaiwa kumvua uanachama Mwakilishi wa
Kiembesamaki, Mansour Yussuf Himid, mwenyewe aimeibuka jana na kusema
anasubiri uamuzi ya vikao vya juu vya chama vilivyoanza jana mjini
Dodoma.
Taarifa kutoka ndani ya kikao cha kamati hiyo
ambazo Mansour amekiri kuzisikia zinaeleza kuwa uamuzi huo umetokana na
yeye kudaiwa kupingana na Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010, ambayo
inaunga mkono muundo wa serikali mbili.
Kwa mara ya kwanza, tuhuma za Mansour zilifikishwa
katika kikao cha Kamati ya Maadili ya CCM Zanzibar, kilichoketi Agosti
16, 2013 katika Ofisi za CCM Kisiwandui ambapo wajumbe wa kamati hiyo
kwa kauli moja walitoka na azimio la kumfuta uanachama mwakilishi huyo.
Uamuzi wa kumvua uanachama Mansour uliwasilishwa
katika kikao hicho chini ya Makamu Mwenyekiti wake ambaye pia ni Rais wa
Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein.
Dk Shein ndiye aliyeongoza kikao hicho, huku
wajumbe wakiwa ni Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai,
Mohamed Hija, Mbaruk Rashid Omari na Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif
Ali Idd, huku mapendekezo ya uamuzi huo yakipelekwa mjini Dodoma kwa
ajili ya uamuzi wa mwisho.
Mambo mengine ambayo anadaiwa kufanya Mansour ni
kuasisi Kikundi cha Kiislamu cha Uamsho ambacho kinadaiwa kuchochea
vurugu visiwani humo.
Akizungumza na gazeti hili Mansour alisema, “Mimi
sina cha ziada ninachosubiri ni uamuzi wa chama. Baada ya uamuzi wa
chama ndiyo nitakuwa na jambo la kuzungumza, tusubiri tu wala tusiwe na
haraka.”
Wakati Mansour akieleza hayo mwasisi wa chama
hicho, Hassan Nassor Moyo alipinga uamuzi huo, akisisitiza kuwa kama
utatekelezwa ni wazi kuwa Mansour atakuwa amenyimwa haki yake ya
kikatiba.
Moyo ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Maridhiano
visiwani humo amesema hata yeye yupo tayari kufukuzwa uanachama kama
ikionekana ana msimamo kama wa mwenzake.
Akizungumza wakati akihojiwa na Idhaa ya Kiswahili
ya Radio Deutsche Welle ya Ujerumani jana, Moyo alisema, “Kama wameamua
kumfukuza siyo sawasawa, wanasema ametofautiana na msimamo au sera ya
CCM ya kuwa na muungano wa serikali mbili, hiyo ni sera ya CCM, lakini
serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na rais wa Zanzibar imetunga
sheria ya mchakato wa Katiba Mpya na imeeleza wananchi, vikundi na
taasisi.”
“Mansour ni sehemu ya watu hao ana haki ya kutoa
maoni yake. Kupanga mikakati ya kumwondoa ndani ya chama ni kumnyima
haki yake ya uraia.”
Alipoulizwa swali na mwandishi wa redio hiyo kuwa
Mansour siyo raia wa kawaida, kwani mbali na kuwa mwanachama wa CCM
aliyeshika nafasi nyingi ndani ya chama hicho na serikali pia ni mjumbe
wa Baraza la Wawakilishi hivyo maoni yake yanaweza kukiathiri chama
alijibu, “Pamoja na kuwa ameshika nafasi za juu za CCM, lakini kubwa ni
kwamba Mansour ni raia, raia ana haki yake ya kutoa maoni tena kisheria
kabisa.”
No comments:
Post a Comment