Wajane JWTZ waililia Serikali
Na Kelvin Lameck
| Sura za Habari Hii |
|---|
| Wajane JWTZ waililia Serikali |
| Chanzo cha vifo |
| MIILI YAWASILI UPANGA |
| Rambirambi |
*Wataka Serikali iwajengee nyumba, isomeshe watoto
*JK kupeleka ombi UN, AU sheria zibadilishwe

Baadhi
ya askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) wakitoa heshima za
mwisho jijini Dar es Salaam jana kwa miili ya askari wenzao waliouawa
Darfur, Sudan, wiki iliyopita. Picha na Anthony Siame
Endelea........WAJANE wa askari saba wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), wameililia Serikali iwasaidie kuwajengea nyumba za kuishi, ili kuepuka matatizo ya kifamilia ambayo yanaweza kuwapata baada ya kufiwa. Mbali ya kuomba msaada huo, wajane hao pia wameiomba Serikali iwasaidie kusomesha watoto wao kutokana na uwezo kuwa mdogo.
Wakizungumza kwa uchungu kwa nyakati tofauti jana, wakati wa kuaga miili saba ya askari hao, katika viwanja vya makao makuu ya JWTZ Upanga, Dar es Salaam, wajane hao wamesema wamebaki katika wakati mgumu wa kukabiliana na maisha.
Mmoja wa wajane hao, Mariam Masudi (30), ambaye aliolewa na marehemu Sajenti Shaibu Salehe Othman na kufanikiwa kuzaa naye watoto wanne, ambao ni Salma Shaibu ambaye anasoma kidato cha nne, Nadhira Shaibu (darasa la sita), Ilham Shaibu (darasa la pili) na Abdulhakim Shaibu (chekechea), akielezea masikitiko yake yakuondokewa na mume wake alisema:
“Nina uchungu sana wa kuondokewa na mwenzangu, nilikuwa namtegemea mume wangu kwa kila kitu.
“Naomba jeshi, linisaidie kusomesha watoto wangu…tumesikia tutapewa fedha, lakini nakwambia nyumba ndiyo itakuwa sehemu ya kutuenzi na watoto wangu,” alisema huku akibubujikwa na machozi.
Naye, mjane Maria Reston (30), ambaye alikuwa ameolewa na Koplo Oswald Chaula alisema anaishi katika nyumba za jeshi katika kota za Chabuluma mkoani Ruvuma, ameachwa na watoto wanne.
“Msiba huu, unaniuma sielewi mume wangu amekufaje jamani, kwa kuwa imetokea namwachia Mungu.
“Taarifa za vifo vya wanajeshi nilizipata kwenye magazeti, sijui kwanini nilihisi mume wangu atakuwa miongoni mwao.
“Niliposoma nikaona jina la mume wangu, siamini kama kweli mume wangu amefariki jamani,” alisema Maria kwa uchungu.
Aliwataja watoto wake, kuwa ni Elizabeth Chaula (anasoma kidato cha kwanza), Clares (darasa la sita), Eliud (darasa la kwanza) na Joshua (ana umri wa miezi 10).
Chanzo cha vifo
Chanzo cha vifo vya askari hao, kinadaiwa kusababishwa na kikundi cha waasi wanaoungwa mkono na kundi la mgambo wa Janjaweed.
Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Jenerali Davis Mwamunyange alisema marehemu waliuawa wakati wakisindikiza walinzi wa amani kutoka eneo la Koabecha kwenda Mesin.
Alisema walitembea kilometa 25, ambapo msafara huo ulipunguza mwendo kutokana na utelezi, ghafla walijikuta wakishambuliwa kwa kushtukiza.
Alisema mashambulizi hayo yalidumu kwa saa mbili, lakini kikosi hicho hakikuwa na silaha nzito kutokana na sheria ya Umoja wa Mataifa kutaka majeshi yanayolinda amani kutokuruhusiwa kufanya hivyo.
RAIS KIKWETE
Kwa upande wake, Rais Jakaya Kikwete amesema atatumia vikao vya UN na Umoja wa Afrika (AU), kuhakikisha sheria zinazotumiwa na majeshi ya kulinda amani katika nchi mbalimbali zinabadilishwa, ili kupunguza vifo vinavyotokana na majeshi ya umoja huo kushambuliwa na adui.
Rais Kikwete ambaye ni Amiri Jeshi Mkuu, alisema umefika wakati wa kutazama upya falsafa ya ulinzi inayotumika katika kulinda amani huko Darfur, kwa sababu eneo hilo sasa ni hatari kwa usalama wa majeshi ya UN.
Alisema hadi sasa, askari zaidi ya 40 wameuawa na 55 kujeruhiwa katika nchi mbalimbali ambazo vikosi vya Umoja wa Mataifa, vimepelekwa kulinda amani.
“Rai hii, tunaipeleka AU na UN, tutahakikisha tunasukuma mbele suala hili kwa ujumla, hali ya sasa kiulinzi si nzuri, tunahitaji kuongeza nguvu ya kujihami, mfumo huu hautufai katika mazingira ya sasa.
“Nilipata taarifa hizi nikiwa Monduli, nilikasirika sana, ninaamini limefanywa na Wasudan wenyewe, kwa nini wawaue watu wetu ambao walikwenda kuwezesha amani ili wao waishi kwa amani?
“Baada ya tukio hili, niliwasiliana na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon na Rais wa Sudan, Omar al- Bashir kwa sababu tukio hili, limefanyika katika mamlaka yake, tunatarajia watafanya uchunguzi wa kutosha kuwabaini na kuwakamata waliohusika.
“Natambua kazi nzuri inayofanywa na askari wetu huko Darfur na kwingineko, nawasihi msikatishwe tamaa, haya yanatukumbusha kila tunapotumwa kulinda amani tuwe na tahadhari zaidi,” alisema Rais Kikwete.
Alisema Tanzania, imekuwa mstari wa mbele kulinda amani katika mataifa mbalimbali, ikiwemo vita ya ukombozi nchini Msumbiji dhidi ya kikundi cha RENAMO ambako askari 90, waliuawa na kuzikwa eneo la Naliendele Mtwara, Liberia (3), Siera Lion, Lebanon, Sudan na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Waziri wa Ulinzi
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha, alisema kuuawa kwa askari wa Tanzania, ni tukio baya na mkakati wa waasi wenye lengo la kukwamisha juhudi za UN na AU kuleta amani.
Alisema wizara yake, itafanya kila jitihada kugharamia familia za marehemu na askari wanaoendelea na matibabu huko Darfur.
MIILI YAWASILI UPANGA
Miili ya askari waliokufa, iliwasili makao makuu ya jeshi Ngome saa 5:15 asubuhi na kushushwa katika magari maalumu na kupokewa kwa heshima za kijeshi hadi eneo lililoandaliwa.
Rais Kikwete ambaye aliongozana na mkewe mama Salma, alikuwa wa kwanza kutoa heshima za mwisho kwa marehemu hao ambapo baadhi ya miili haikuweza kufunguliwa kutokana na sababu za dini.
Wakati wa kuaga miili hiyo, simanzi kubwa ilitawala eneo lote la jeshi, ambapo mmoja wa askari wa kike mbaye hakufahamika jina lake, alianguka na kupoteza fahamu mbele ya jeneza la marehemu, Sajini Shaib Salehe Othman.
Viongozi wengine, walioshiriki kuaga miili ya askari hao ni pamoja na Makamu wa Rais, Dk. Mohamed Gharib Bilal, Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar, Seif Ally Idd, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi, Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahaman Kinana, Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Said Mwema, maofisa wa ngazi wa vikosi vya ulinzi na usalama na wananchi.
Rambirambi
Wakati huo huo, Kaimu Mkurugenzi wa Habari na Mahusiano wa JWTZ, Meja Joseph Masanja alisema, Jumuiya ya Watanzania wanaoishi Sudan pamoja na askari wanaoendelea kulinda amani, wametoa Dola za Marekani 700, Umoja wa Mataifa wao wametoa Dola 1,800 ambazo ni sawa na Sh milioni 2,880,000 pamoja na medali ili kutambua na kuthamini kazi za marehemu hao.
Alisema JWTZ, watafanya utaratibu wa namna fedha hizo pamoja na medali zitakavyowafikia warithi wa marehemu.
No comments:
Post a Comment