WAZEE 292 WAPATIWA VITAMBULISHO VYA MATIBABU
Kushoto ni Afisa mtendaji kata ya
Utengule Usongwe wilaya ya Mbeya Vijijini mkoani MBEYA, John
Mwanampazi, akiwa na Afisa Maendeleo ya Jamii kata hiyo Martin Gowele
wakizungumza na mwandishi wa habari.
Na, Kelvin Lameck, Mbalizi
Ili kutekeleza sera ya taifa ya wazee ya mwaka 2003 inayosema wazee
kuanzia miaka 60 watapata huduma za afya bure, Halmashauri ya wilaya ya Mbeya
Vijijini, imeanza kuwapatia wazee vitambulisho vya kudumu vya matibabu.
Katika kata ya Utengule Usongwe yenye vijiji sita, wazee 292 tayari
wamepatiwa vitambulisho hivyo ambavyo vitawawezesha kutibiwa bure maisha yao
yote katika hospitali za serikali ndani ya mkoa wa Mbeya.
Wakizungumza na Mtandao wa Meck lameck.blogspot.com ofisini kwao, Ofisa mtendaji wa kata hiyo John
Mwanampazi na ofisa Maendeleo ya jamii wa kata Martin Gowele, walisema kuwa
awamu ya kwanza waliwapatia wazee192 na awamu ya pili wazee 80.
‘’Tuliwatangazia viongozi wa serikali za vijiji kuwa wazee wote wenye
umri wa kuanzia miaka 60 wanapaswa kuleta picha moja ya Passport ambapo
anatengenezewa kitambulisho cha matibabu’’ alisema Gowele.
Alisema wazee wengi wamejitokeza na baadhi wameanza kufurahia matibabu
wanayopata bure kupitia vitambulisho hivyo.
Kwa upande wake, Ofisa Mtendaji wa kata hiyo John Mwanampazi, alisema
kijiji kinachoongoza kwa wazee wengi kujitokeza kupatiwa vitambulisho hivyo ni
Kijiji cha Mbalizi.
‘’Mbalizi inaongoza na ninawataka wazee wote wenye kuanzia miaka 60
wajitokeze kuja kujiandikisha na kuchukua vitambulisho vya matibabu maana ni
mpango wa serikali na vinatolewa bure’’ alisema Mwanampazi.
Alivitaja vijiji vilivyopo katika kata hiyo kuwa ni Mbalizi, Utngule,
Idugumbi, Itimba, Iwala na Ihombe.


No comments:
Post a Comment