Pages

Thursday, 18 July 2013

  Mbeya

TAMASHA LA INJILI KUWEKA HISTORIA MBEYA


TAMASHA kubwa la muziki wa injili linalotarajiwa kufanyika ukumbi wa Kanisa la Pentekoste Holiness Association Mission (Makimbilio), karibu na lango kuu la Shule ya Sekondari Samora, Mbeya Agosti 4, mwaka huu, linatarajiwa kuweka historia mpya.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Mratibu wa tamasha hilo, George Kayala alisema kuwa, wasanii mbalimbali wa Bongo Movie wakiongozwa na pacha wa muigizaji wa filamu na muziki, Husna Posh 'Dotnata', Dometria Alphonce 'DD' wameandaa kitu kwa ajili ya wakazi wa Mbeya.

“Tamasha hilo litakuwa ni la kihistoria, kwani litapambwa na wasanii wa filamu nchini wakiongozwa na pacha wa Dotnata na watakuwa na jambo la kusema na watu watakaofika katika tamasha hilo,” alisema Kayala.

Kayala alisema kuwa tamasha hilo limeandaliwa na GMK Production kwa ajili kuitambulisha albamu ya tatu ya ‘Nitang’ara Tu’ ya Mwinjilisti Kabula George, ikiwa katika mfumo wa DVD na siku hiyo itauzwa kwa wakazi wa Mbeya.

Kiingilio katika tamasha hilo ni sh 2,000 kwa watu wazima na 1,000 kwa watoto na shughuli itaanza saa 7:00 mchana na kumalizika saa 12:00 jioni.

“Tumeamua kuweka kiingilio kidogo ili kila mmoja apate kuingia katika tamasha hilo, ambalo litakuwa la kwanza kuwakutanisha nyota wa filamu na waimbaji wa nyimbo za injili mkoani humo,” alisema Kayala.

Tamasha hilo limedhaminiwa na Ushindi Redio FM ya Mbeya, Shalom Production, DD Entertainment, The Genesis Global College na Dotnata Entertainment.

No comments:

Post a Comment