MRADI mkubwa wa ujenzi wa Soko jipya la Mwanjelwa ulioanza baada
ya soko lililokuwapo kuteketezwa kwa moto mwaka 2006, umekwama
kumalizika kutokana na mkandarasi aliyepewa kazi hiyo kuishiwa fedha.
Uchunguzi wa umebaini kukwama kwa ujenzi wa soko hilo
katika hatua za mwisho huku timu ya wataalamu kutoka Benki ya CRDB
iliyotoa mkopo wa sh bilioni 13 wakihaha kufuatilia deni lao.
Benki ya CRDB iliikopesha Halmashauri ya Jiji la Mbeya fedha hizo ili
kufanikisha ujenzi wa soko hilo na mkopo ulitakiwa utumike ndani ya
miaka mitano na baada ya hapo jiji hilo lianze kurejesha mkopo huo na
riba.
Kushindwa kukamilika kwa soko hilo ambalo ni kitega uchumi kikubwa
katika halmashauri ya jiji hilo kumeibua hisia tofauti huku baadhi ya
wafanyabiashara wakilalamikia uzembe uliofanywa na mkandarasi, Kampuni
ya Tanzania Building Works Ltd (TBWL).
Mkurugenzi wa Tawi la CRDB Mbeya, Benson Mwakyusa, alisema ingawa si
msemaji alikiri kupokea ugeni kutoka CRDB makao makuu na kwamba walikuwa
na jukumu la kufuatilia masuala mengine ya kikazi na kukutana na
mkopaji ambaye ni halmashauri ya jiji hilo, ili kuangalia njia nyingine
ya kukamilisha ujenzi wa soko hilo.
Mhandisi mshauri wa ujenzi wa soko hilo, Dudley Mawalla, kutoka
Kampuni ya MD Consultancy Limited alipohojiwa ili aeleze hali
iliyosababisha ujenzi wa soko hilo usimame, naye aliruka na kudai kuwa
si msemaji na anayetakiwa kusema ni mmiliki wa soko hilo ambao ni Jiji
la Mbeya.
Mkurugenzi wa jiji hilo, Musa Zungiza, alikiri mkandarasi aliyepewa
kazi ya ujenzi wa soko kushindwa kumalizia ujenzi licha ya kuomba
aongezewe muda ambao nao ulimalizika na ndipo walipogundua kuwa
aliishiwa fedha na ameshindwa pia kutimiza masharti waliyokubaliana.
“Sisi kama jiji hatumdai hadi pale alipofikia, kweli alituomba fedha,
tulimuomba atupatie mpango mzima wa kazi na mtiririko wa fedha kutoka
benki, tumefikia mahali tumekosana kwa kuwa hajatimiza masharti na
tumezungumza na mhandisi mshauri ili tuone jinsi ya kumpata mkandarasi
mwingine,” alisema Zungiza.
|
No comments:
Post a Comment