Mwandosya amuita Lowassa kambi yake
Profesa Mark Mwandosya, ambaye anawania kuteuliwa na CCM kugombea urais, amemtaka Edward Lowassa kujiunga na kambi yake kwa kuwa makada wengine wanne kwenye mbio hizo wanamuunga mkono.
Hata hivyo, wawili kati ya makada hao wanne wamekana kumuunga mkono.
Mwandosya, ambaye ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais
(Kazi Maalum), alisema tayari Waziri Mkuu Mizengo Pinda, Waziri wa
Kilimo na Maendeleo ya Mifugo, Steven Wasira, Waziri wa Uchukuzi, Samuel
Sitta na waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard
Membe wanamuunga mkono na hivyo kumshauri Lowassa kujiunga na kambi
yake.
“Kama (wagombea) wengi wananiunga mkono,
aliyebakia basi atakuwa ni ndugu yangu, rafiki yangu, Edward Lowassa.
Naye angesema hivyo ingerahisisha sana kazi ya chama, ingepunguza sana
kazi, makundi yangekuwa yameisha,” alisema Mwandosya baada ya kurejesha
fomu za kuomba CCM impitishe kugombea urais.
“Halmashauri Kuu isingepata shida, Kamati Kuu
isingepata shida nadhani tungeweza kufika pale ambako tungefika tarehe
12 (Julai, siku ambayo Mkutano Mkuu wa CCM utamchagua mgombea urais),
bila kikwazo, bila makundi,”alisema mbunge huyo wa Rungwe Mashariki
jana.
Lakini kauli yake imepokewa kwa hisia tofauti na
watu hao aliodai wanamuunga mkono, huku kambi ya Lowassa ikizungumzia
kauli hiyo kuwa si ya mtu aliye makini kwenye mbio za urais.
Jumla ya makada 40 wamechukua fomu za kuomba
ridhaa ya CCM kugombea urais katika Uchaguzi Mkuu uliopangwa kufanyika
Oktoba 25 na chama hicho kina kazi ngumu ya kumpata mwanachama
atakayemrithi Rais wa sasa, Jakaya Kikwete ambaye katiba inamzuia
kuendelee kuongoza baada ya kumaliza vipindi viwili vya miaka mitano
kila kimoja.
Mgombea urais wa CCM pia ndio atakuwa mwenyekiti wa chama hicho.
Akizungumza mara baada ya kurudisha fomu jana,
Profesa Mwandosya alisema mchakato huo umewafanya wanaoomba urais kuwa
marafiki zaidi licha ya kupigana vijembe, akisema ingekuwa nchi nyingine
wangefanyiana vurugu.
Aliwashukuru wagombea wenzake waliotamka hadharani
kuwa watamuunga mkono endapo hawatapitishwa na Kamati Kuu ya CCM
kugombea urais.
“Namshukuru Benard Membe ambaye ametangaza na
kuandikwa (kwenye vyombo vya habari) kwamba yeye ameona katika orodha
yote ya watu 40, kama si yeye basi ataniunga mkono mimi na yupo tayari
kuzunguka nchi nzima iwapo chama kitaniteua kuwa mgombea,” alisema
Profesa Mwandosya.
“Namshukuru pia Mheshimiwa Pinda, amelizungumzia
hili katika vituo kama si kimoja viwili kuwa moyo wake utakuwa na furaha
kama Profesa Mwandosya anaweza kuteuliwa na chama.”
No comments:
Post a Comment