Ni vilio vitupu A. Kusini
Mjane wa Rais wa Kwanza Mazalendo wa Afrika Kusini, Graca Machel akitoa
heshima za mwisho kwa mwili wa mumewe katika Ikulu ya Pretoria nchini
humo jana. Picha na AFP
Pretoria: Familia ya Rais wa kwanza mzalendo wa Afrika Kusini,
Nelson Mandela jana iliongoza utoaji wa heshima za mwisho kwa mwili wa
kiongozi huyo, katika tukio ambalo limebadili mwelekeo wa maombolezo
tangu alipofariki dunia, Desemba 5, mwaka huu.
Mjane wa Mandela, Graca Machel aliwaongoza
wanafamilia katika Ikulu ya Pretoria waliposema ‘buarini’ kwa kiongozi
huyo katika tukio ambalo mbali na kufungua pazia ya utoaji wa heshima za
mwisho, liliibua simanzi miongoni mwa waliohudhuria.
Mandla ambaye ni mjukuu mkubwa wa Mandela, yeye
alikuwa katika Majengo ya Umoja ilipo Ikulu tangu asubuhi na
alikabidhiwa mwili kama kiongozi wa familia kutoka kwa Majenerali wa
Jeshi la Afrika Kusini (SADF).
Mandla akionekana mwenye mawazo mengi na huzuni
kubwa, kutwa nzima alikuwa ameketi pembezoni mwa jeneza lililokuwa na
mwili wa babu yake, hadi ulipoondolewa Ikulu na kwenda kuhifadhiwa
katika Hospitali ya Jeshi saa 11:30 jioni. Wakati familia ya Mandela
ikiingia kuaga, jeneza lilikuwa wazi likiacha kioo pekee kilichokuwa
kikiwatenganisha na mwili wa mpendwa wao.
Graca alikuwa hatua chache nyuma ya Rais Jacob
Zuma na alipofika katika jeneza lenye mwili wa mumewe alisimama kwa
sekunde chache akimtazama, kisha akaendelea. Nyuma ya Graca, alikuwa ni
Mtalaka wa Mzee Mandela, Winnie Madikizela na mabinti zake wawili,
pamoja na wanafamilia wengine, ambao baada ya kutoa heshima zao za
mwisho, walionekana wakitumia lesso zao kufuta machozi. Familia hiyo
ilifuatiwa na Rais Mstaafu, Thabo Mbeki na Frederick de Klerk ambao
waliambatana na wake zao, lakini mke wa de Klerk, Elita alishindwa
kujizuia na kuangua kilio.
Kulikuwa na simanzi kubwa miongoni mwa
waombolezaji waliofika kutoa heshima zao za mwisho, wakati ambao Rais
Zuma pia aliwaongoza viongozi wa nchi mbalimbali kumuaga Madiba.
Rais Jakaya Kikwete alikuwa miongoni mwa waliotoa
heshima za mwisho akiungana na marais wenzake, wengi wakiwa kutoka
Afrika ambao waliondoka jana mchana baada ya kupata fursa hiyo.
Miongoni mwao walikuwa marais wastaafu; Kenneth Kaunda wa Zambia na Joachim Chissano wa Msumbiji.
Marais wengine waliokuwapo na nchi zao kwenye
mabano ni Robert Mugabe (Zimbabwe), Joyce Banda (Malawi), Uhuru Kenyatta
(Kenya), Ellen Johnson – Sarlief (Liberia), Goodlucky Jonathan
(Nigeria) na Michael Satta (Zambia).
Jeneza lenye mwili wa Mandela liliwekwa juu ya
kizimba maalumu ambacho kilikuwa kimezungushiwa utepe wenye rangi
nyekundu, huku ukiwa umefunikwa na kibanda cha rangi nyeupe
kilichojengwa kwa ustadi mkubwa.
Walikuwapo askari wanne wa Kikosi cha Jeshi la
Wanamaji wa Afrika Kusini wakizunguka jeneza hilo; wawili mwanzoni na
wawili mwishoni, wakiwa wamevalia mavazi meupe, kushika kitara mkononi
kila mmoja.
No comments:
Post a Comment