Pages

Sunday, 8 December 2013

Ibada maalumu ya Mandela


Rais wa Kwanza mzalendo wa Afrika Kusini,Nelson Mandela. 

Johannesburg. Afrika Kusini, jana ilitawaliwa na ibada na maombi yaliyofanyika katika makanisa mbalimbali kuliombea taifa, baada ya kifo cha Rais wa Kwanza mzalendo, Nelson Mandela.
Rais Jacob Zuma alikuwa miongoni mwa waumini wa Kanisa la Bryanston Methodist, Johannesburg katika ibada ambayo pia ilihudhuriwa na mtalaka wa Mandela, Winnie Madikizela pamoja na mjukuu mkubwa, Mandla.
Ibada za aina hiyo ziliendeshwa kila kona ya nchi, zikiwaweka pamoja Waafika Kusini ambao waliitikia wito wa Rais Zuma wa kuitumia Jumapili kuliombea taifa hilo.
Nyimbo za dini zilisikika katika kumbi za ibada na makanisa, ambako viongozi wa Serikali wakiwamo Naibu Rais wa Afrika Kusini, Kgalema Motlante na Rais Mstaafu, Thabo Mbeki walikuwa miongoni mwa waliopangiwa kushiriki katika ibada hizo.
Katika Kanisa la Baptist, baadhi ya waumini wakiwa katika mavazi rasmi walionekana wakiimba na kucheza, kabla ya Rais Zuma kupewa nafasi ya kuzungumza.
“Kwa nchi yetu, kifo cha Baba Madiba ni hasara ya aina yake. Waafrika Kusini tunapaswa kuomba tukikumbuka mambo mema ya kiukombozi na uhuru, amani, msamaha, haki na kujali ambayo Mandela aliyapigania na kuyasimamia,” alisema Zuma.
Kwa upande mwingine, mamia ya wafuasi wa Chama cha African National Congress (ANC), walifurika katika Ukumbi wa Benki ya Standard, Johannesburg kushiriki katika maombi, wakiitikia wito wa Rais Zuma.
Mwandishi wetu alishuhudia makada wa chama hicho wakiwa katika mavazi rasmi, wakicheza muziki wa Injili na baadaye wakishiriki maombi yaliyowahusisha waumini wa madhehebu ya Kikristo, Kiislamu, Kihindu, Kiyahudi, Bahai na wale wanaoamini katika imani za jadi.
Qunu kimya
Wakati nyimbo na ngoma zikichezwa kwa ajili ya kusifu kazi alizofanya Mandela, katika Kijiji alichokulia Qunu, eneo la Mthatha kuliripotiwa kuwa kimya huku wakazi wake wakikataa kuzungumza na waandishi wa habari kuhusu kifo cha Mandela.
Wanakijiji hao wameamua kukaa nyumbani wakiomboleza na inaaminika kwamba wengi hawaamini kilichotokea na pengine wanasubiri kushuhudia mwili wa kiongozi huyo utakapofikishwa huko Jumamosi kwa ajili ya mazishi yatakayofanyika Jumapili.

No comments:

Post a Comment