Pages

Sunday, 20 October 2013

Utafiti wabashiri Katiba mpya

WAKATI Tume ya Mabadiliko ya Katiba ikiandaa rasimu ya pili ya Katiba itakayopelekwa katika Bunge la Katiba, utafiti uliofanywa na asasi ya kimataifa umebashiri baadhi ya matokeo ya Katiba ijayo.

Utafiti huo uliofanywa na taasisi ya kimataifa ya Afro Barometer kwa kushirikiana na Asasi ya Utafiti Kuhusu Uondoaji Umasikini (Repoa), umeelezea namna Watanzania wanavyouangalia Muungano na wanavyotaka uwe.
Kwa mujibu wa matokeo ya utafiti huo yaliyotangazwa mwishoni mwa wiki, Watanzania pamoja na mambo mengine, walitakiwa watoe maoni kuhusu muundo wa Muungano wanaoutaka.
Kati ya wahojiwa waliochaguliwa bila kufuata upendeleo wowote kutoka katika kila pembe ya nchi, asilimia 42 walisema wanataka muundo wa Muungano uliopo, ambao ni wa Serikali mbili uendelee kama ulivyo, huku asilimia 21 wakisema uwe wa Serikali tatu.
Asilimia 13, wametaka Muungano wa serikali moja, asilimia kumi Muungano uvunjwe na ni asilimia nane tu ndio waliotaka Zanzibar iongezewe uhuru na madaraka ndani ya Muungano.
Walipoulizwa kama wanakubali Waziri asitoke ndani ya Bunge ili kutekeleza vyema kanuni ya mfumo wa kutenganisha majukumu ya Serikali na ya Bunge, asilimia 54 ya wahojiwa walitaka mawaziri wasiteuliwe kutoka miongoni mwa wabunge.
Aidha asilimia 42 walipendekeza mawaziri waendelee kuteuliwa kutoka miongoni mwa wabunge, kwa madai kuwa mfumo huo hauathiri kanuni hiyo.
Maandamano
Aidha msimamo wa mara kwa mara ya Jeshi la Polisi nchini kuruhusu mikutano ya hadhara kufanyika bila kutanguliwa na maandamano ya kisiasa, imeungwa mkono na maoni ya Watanzania wengi waliohojiwa katika utafiti huo, huku sehemu kubwa wakionesha hawapendi maandamano ya siasa yanayoambatana na vurugu.
Watanzania walipoulizwa kama wamewahi kishiriki katika maandamano kudai au kupinga jambo na kama wako tayari kushiriki, wengi walipinga.
Katika swali hilo, asilimia 62 ya wahojiwa walisema hawajawahi kushiriki maandamano na hawatashiriki maandamano huku asilimia 22 wakisema hawajashiriki, lakini wanaweza kushiriki wakipata nafasi.
Ni asilimia kumi tu ya wahojiwa walisema kuwa wameshiriki mara kwa mara huku asilimia sita ya wahojiwa wakisema wameshiriki mara moja au mbili.
Mbali na maandamano, Watanzania pia walipohojiwa kama wako tayari kutumia mabavu au vurugu kwa sababu za kisiasa, asilimia 88 walisema hawako tayari kushiriki katika siasa za aina hiyo.
Walipotakiwa waelezee kama wanakubaliana au wanapinga dhana kwamba Polisi wana wajibu wa kulazimisha wananchi watii sheria, asilimia 78 ya wahojiwa walikubaliana na dhana hiyo, huku asilimia 20 wakipinga.
Jeshi litawale
Hata hivyo walipoulizwa kama wanakubaliana na dhana ya Jeshi kushika madaraka na kutawala, asilimia 18 ya Watanzania walielezea kukubali mfumo huo wa utawala, huku asilimia 79 wakipinga utawala wa aina hiyo.
Walipohojiwa kama wanakubali mfumo wa chama kimoja ambao ulikuwepo kabla ya 1992, asilimia 22 waliunga mkono mfumo huo, huku asilimia 76 wakipinga.
Kuhusu kama Tanzania ina utawala wa demokrasia, walipoulizwa watoe maoni, asilimia 76 wamekubali kuwa Tanzania inayo demokrasia yenye matatizo madogo huku asilimia tatu tu wakisema hakuna demokrasia.
Wahojiwa walipoulizwa kama wanaridhika na namna demokrasia inavyofanya kazi nchini, asilimia 75 walisema wanaridhika huku asilimia 22 wakisema hawaridhiki.
Wananchi hao asilimia 72 walisema wananchi wanapaswa kuwa makini ikibidi kutoziamini kauli za wanasiasa mara kwa mara huku asilimia tano wakisema hakuna haja ya kuwa makini nazo.
Ukabila
Katika utafiti huo, wahojiwa walipotakiwa waseme nini kati ya kabila lao na Utanzania wao wanachojisikia vizuri kujitambulisha nacho, asilimia 61 ya Watanzania walisema ni Utanzania tu unaowatambulisha vizuri na hawawezi kabisa kuulinganisha na kabila lao.
Asilimia sita walisema wanajisikia vizuri zaidi kujitambulisha kwa Utanzania wao lakini hawaoni ubaya kujitambulisha kwa kabila lao huku asilimia 29 wakisema kabila lao na Utanzania wao vyote vinawatambulisha vizuri.
Kati ya wahojiwa hao, asilimia moja walisema wanajisikia vizuri zaidi kutambulishwa kwa kabila tu, huku asilimia tatu wakisema wanajisikia vizuri kutambulishwa kwa kabila lao kuliko Utanzania wao.

No comments:

Post a Comment