Pages

Monday, 7 October 2013

Mbunge ajitoa ujumbe bodi ya CDA kupinga bomoabomoa

 mji fa4dc
NA JACQUELINE MASSANO
Mbunge wa Dodoma Mjini, David Malolle (CCM), ametangaza rasmi kujitoa kwenye ujumbe wa Bodi ya Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA) na kuwataka wananchi kuandamana ili mamlaka hiyo ifutwe kwani imekuwa ikibomoa mji na si kuuboresha.(hd)

Mbunge huyo alitoa kauli hiyo juzi alipokuwa akizungumza na wananchi wa Kata ya Chang'ombe Magharibi mara baada ya uzinduzi wa ofisi ya tawi la kata hiyo.
"Mimi binafsi sioni sababu ya kuendelea kuwapo ndani ya bodi hiyo wakati wananchi wangu wanaendelea kunyang'anywa mashamba, viwanja na kuvunjiwa nyumba bila sababu za msingi," alisema na kuongeza:
"Hata CDA inapochukua eneo kubwa la mwananchi wangu hawako tayari kumuachia viwanja zaidi ya kimoja na wala fidia hawawalipi sasa kwa nini mimi niendelee kukaa ndani ya hiyo bodi."
Malolle alisema licha ya kuwapo katika bodi hiyo, lakini ushauri wake umekuwa ukipuuzwa, hivyo haoni sababu ya kuendelea kuwapo ndani ya bodi. Alisema kutokana na kuendelea kwa hali hiyo ni muhimu sasa wananchi wa meeneo yote wanaotishiwa kuvunjwa na mamlaka hiyo kuandamana ili kuhakikisha bodi hiyo inavunjwa.
Aidha, alisema kutokana na yeye kutokuwa mjumbe tena kwenye bodi hiyo, yupo tayari kukunjua makucha ili kuhakikisha CDA inafanya kazi iliyokusudiwa na si vinginevyo.
"Kusudio la serikali kuanzisha Bodi hiyo ni kuhakikisha kuwa mji wa Dodoma unaboreshwa na si kubomolewa na wenyeji kuhamishwa kwa madai ya kupanga mji...sasa kama kazi ya CDA ni kubomoa mji kwa kisingizio cha ujenzi wa makao makuu, nawaomba wakazi wenzangu wa Nzunguni, Miyuji na sehemu zingine tuungane pamoja tuandamane kuipinga mamlaka hii," alisema.
Kwa mujibu wa mbunge huyo, CDA imekuwa ikivunja sehemu mbalimbali na wanapoulizwa na wananchi hudai kuwa wakamuulize mbunge kwani ni mjumbe wa bodi ambaye anajua kilichoamuriwa, jambo ambalo alisema siyo kweli.
Naye, Katibu wa CCM Mkoa wa Dodoma, Albert Mgumba, alisema wale wote wanaoleta msuguano ndani ya chama wakati wa chaguzi watolewe mapema. Alisema sehemu nyigi ambazo CCM ilikosa udiwani au ubunge katika chaguzi zilizopita kulisababishwa na wana-CCM wenyewe, hivyo hakuna sababu ya kuwalea watu wa aina hiyo.
"CCM ndiyo chama pekee ambacho kimeweza kutunza amani na utulivu katika kipindi chote cha Uhuru wa Tanzania... bila nia njema ya waasisi wa nchi akiwamo Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere na Karume, amani iliyopo hivi sasa isingekuwapo," alisema.

No comments:

Post a Comment