Wakurugenzi 70 vinara mtandao wa ufisadi
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda
Kwa ufupi
Dar es Salaam. Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), imebaini mtandao wa ufisadi unaoshirikisha wakurugenzi 70 wa halmashauri mbalimbali hapa nchini ambao wanashirikiana na baadhi ya watendaji wa Ofisi ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) na Kitengo cha Hazina.
Baadhi ya halmashauri hizo ni pamoja na Wilaya ya Monduli, Arusha, Mwanza, Mbeya na Ilala.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es
Salaam jana, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Rajab Mohamed Mbarouk alisema
keshokutwa atataja majina ya wakurugenzi hao ili wananchi waweze
kuwafahamu.
Mbarouk alisema kuwa Tanzania Bara ina halmashauri
134, kwa hiyo ina maana zaidi ya nusu ya wakurugenzi wanajihusisha na
mambo hayo.
“Baadhi ya wakurugenzi hao walihamishwa kwenye
vituo vyao vya kazi kutokana na kashfa ya matumizi mabaya ya fedha za
Serikali, lakini bado wanajihusisha na mambo haya,” alisema Mbarouk.
Alisema kutokana na hali hiyo, kamati hiyo
imepanga kukutana kesho na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na Waziri wa
Tamisemi, Hawa Ghasia ili kuzungumzia suala hilo.
“Kuna zaidi ya wakurugenzi 70 wako kwenye mtandao
wa ufisadi kwa kushirikiana na watendaji wa Hazina na Tamisemi, jambo
ambalo limesababisha halmashauri zao kupata hati chafu kwa miaka mitano
mfululizo,”alisema Mbarouk.
Aliongeza wakurugenzi hao wamekuwa wakishirikiana
na wahasibu wao katika kutumia vibaya fedha za Serikali zinazotolewa kwa
ajili ya kuendeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika halmashauri
zao.
Akitolea mfano wa Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza,
Wilson Kabwe ambapo halmashauri yake imefanya vibaya katika ripoti ya
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), lakini
hajachukuliwa hatua na badala yake amekuwa Mkurugenzi wa Jiji la Dar es
Salaam.
Alisema mbali na halmashauri hiyo, aliyewahi kuwa
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo, Rhoda Nsemwa ambaye
alisimamishwa kazi kutokana na tuhuma za ufisadi, lakini bado anaendelea
kupata mshahara na stahiki zake kama mtumishi aliye kazini.
“Tumeshangaa kuona kuwa, aliyekuwa Mkurugenzi wa
Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo bado anaendelea kulipwa mshahara, kodi
ya nyumba na marupurupu mengine kama ofisa aliye kazini wakati ana kesi
ya matumizi mabaya ya fedha za Serikali,” alisema.
Alibainisha kamati hiyo pia imebaini kuwa Takukuru
inajihusisha moja kwa moja na vitendo vya rushwa, kutokana na kupotosha
ukweli wa taarifa za watuhumiwa na kuchelewesha kuwasilisha jalada
mahakamani.
No comments:
Post a Comment